Makumi ya maelfu ya Wasomali wamejitokeza mitaani kote nchini Somalia siku ya jana Jumanne Disemba 30, wakipinga uamuzi wa Israel kuitambua Somaliland, eneo lililojitangaza kujitenga ambalo Somalia inalichukulia kuwa sehemu ya eneo lake la mamlaka ya kitaifa.
Umati mkubwa ulikusanyika katika mji mkuu Mogadishu, ndani ya uwanja wa taifa, ambako viongozi wa kidini waliongoza maandamano yaliyotoa wito wa umoja wa kitaifa na kulaani hatua hiyo wakisema ni shambulio dhidi ya uhuru na umoja wa ardhi ya Somalia.
Maandamano kama hayo pia yaliripotiwa katika miji ya Baidoa, Guriel, Dhusamareeb, Las Anod na Buhoodle, ambapo waandamanaji walibeba bendera za Somalia na kupiga kaulimbiu za kupinga kutambuliwa kwa Somaliland.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Somalia, Abdisalam Abdi Ali, ameonya kuwa uamuzi wa Israel unaweza kusababisha athari kubwa katika ukanda mzima. Alisema hatua hiyo inatishia usalama katika Pembe ya Afrika na maeneo ya jirani, yakiwemo Bahari Nyekundu na Ghuba ya Aden, na inaweza kuwapa nguvu makundi yenye misimamo mikali yanayoendesha shughuli zake katika eneo hilo.
Huko Las Anod, waandamanaji wameelezea maandamano hayo kama ishara ya mshikamano wa kitaifa wakisema wanapinga aina yoyote ya uchokozi kutoka kwa serikali ya Israel, hasa kutoka kwa Benjamin Netanyahu na harakati zake za Kizayuni.
Somaliland ilitangaza kujitenga na Somalia mwaka 1991, lakini haikuwa imetambuliwa rasmi na nchi yoyote hadi wiki iliyopita. Tangu wakati huo, zaidi ya mataifa 20 yameilaani hatua ya Israel. Somalia pia iliwasilisha suala hilo katika kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ikidai kuwa kutambuliwa huko kunahatarisha uthabiti wa kanda, madai ambayo Israel imeyakataa.
