Monday , 9th May , 2016

Naibu waziri wa Ofisi ya Rais TAMISEMI utumishi na utawala bora Suleiman Jafo amesema kwamba serikali inayoongozwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) haifanyi mambo ya kanyaga twende bali inajitahidi kuleta huduma bora kwa wananchi.

Jafo ameyasema hayo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Riziki Shahali Mngwali (CUF) aliyetaka kujua ni kwa nini serikali inaendelea kuwaajiri wakunga wanaume ambao huwazalisha wanawake jambo ambalo ni udhalilishaji kwa wanawake.

Akijibu swali hilo Jafo amesema kwamba serikali itaendelea kuwaajiri wakunga wanaume na wananwake kwa kuwa wote wamefundishwa maadili ya kazi kutoka baraza la wakunga na vilevile hufanya kazi kwa mujibu wa sheria ya ya ukunga ya mwaka 2010.

Aidha Naibu Waziri Jafo amesisitiza kwamba kutafanyika utafiti katika maeneo ambayo mila na desturi zao zinawanyima uhuru kuweza kuhudumiwa na wanaume wakati wa kujifungua ili serikali iweze kuwapanga wanawake wakunga katika maeneo hayo.