
Mbunge wa jimbo Bunda mjini, Esther Bulaya, leo amewashinda Mahakamani wakazi wanne wa jimbo hilo waliofungua kesi ya kupinga ushindi alioupata katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana, baada ya kumshinda mpinzani wake, Stephen Wasira, aliyetetea kiti hicho kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Katika kesi hiyo, Bulaya mbunge aliyeshinda uchaguzi kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alikuwa akitetewa na mwanasheria maarufu nchini, Tundu Lissu huku watuma maombi wakitetewa na Constantine Mutalemwa.
Akitoa maamuzi wa kuitupiliambali kesi hiyo katika Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Jaji Gwae, amedai walalamikaji katika kesi hiyo hawana mamlaka kisheria kufungua kesi hiyo wala hawakuna sehemu waliyoonyesha kuathirika na uchaguzi huo.
Kesi hiyo ya uchaguzi namba 1 ya mwaka 2015, mjibu maombi wa kwanza (Bulaya), alikuwa akishitakiwa na Magambo Masato, Matwiga Matwiga, Janes Ezekiel na Ascetic Malagira, ambao walikuwa na mawakili wawili ambao ni Mutalemwa na Denis Kahangwa.
Aidha, watuma maombi hao walikuwa wakimlalamikia msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo ambaye ni mjibu maombi wa pili na mwanasheria mkuu wa serikali, ambao wote walikuwa wakitetewa na wakili Paschal Malongo.
Baada ya Mahakama kutupilia mbali kesi hiyo Mbunge huyo wa Bunda Mjini Ester Bulaya amesema alishinda uchaaguzi kwa halali na sasa yupo tayari kuendelea na majukumu ya kuwatumikia wananchi.
"Nilimshinda Wasira kwa wananchi, na leo nimemshinda kisheria, Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza imetupilia mbali kesi ya Uchaguzi dhidi yangu, iliyofunguliwa na wapambe wa Wasira. Mungu husimama na watu walio wema. Nakutumaini mungu wangu na wewe ndiye mlinzi wangu''
''Asante sana wananchi wangu wa Bunda Mjini mliokwenda Mwanza kusikiliza hukumu. Mbunge wenu nipo Dodoma tayari kwa kuanza vikao vya Bunge Kesho". Alisema Bulaya