Wednesday , 12th Oct , 2016

Nchi ya Japan kupitia Shirika lake la Maendeleo, (JICA), limeahidi kuongeza kiwango cha ruzuku kwa serikali ya Tanzania ili kufadhili miradi mbalimbali ikiwemo ile ya Kilimo, Miundombinu ya barabara na huduma nyingine za kijamii.

Makamu wa Rais wa Shirika la Maendeleo la Japan-JICA, Hiroshi (Hiro) Kato, akimfafanulia jambo Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango.

Ahadi hiyo imetolewa na Makamu wa Rais wa Jica, Hiroshi Kato, alipokutana na kufanya mazungumzo na waziri wa fedha na mipango, Dkt. Philip Mpango jijini Washington DC, nchini Marekani.

Kato amesema kuwa Tanzania na Japan ni marafiki wa muda mrefu hivyo nchi itaendelea kuifadhili Tanzania kwa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo itakaoyasaidia kukuza uchumi na kuboresha maisha ya Watanzania.

Aidha ameongeza kuwa Japan imeongeza pia kiwango cha ufadhili kwa bara la Afrika kutoka dola milioni 13 za kimarekani ambazo nchi hiyo ilikuwa ikitoa hadi kufikia dola elfu 30 kwa mwaka kuanzia mwezi Agosti mwaka huu kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo.

Kwa upande wake Waziri wa Fedha , Dkt. Philip Mpango ameishukuru serikali ya Japan kwa kuisaidia Tanzania katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kijamii.

Amesema kuwa miradi inayofadhiliwa na serikali ya Japani ni pamoja na barabara ya Arusha, Holili, Taveta hadi nchini Kenya, pamoja na ujenzi wa bara bara za Juu(Flyover) eneo la Tazara ili kupunguza msongamano jijini Dar es Salaam.