Monday , 22nd Feb , 2016

MAHAKAMA kuu kanda ya Iringa imetoa siku nne kwa walalamikiwa kumpa majibu wakili wa upande wa mashitaka katika kesi ya kupinga matokeo ya mwaka 2016 iliyoanza kusikilizwa jana mkoani Njombe.

Amri hiyo inakuja baada ya wakili wa mshitaki Emmanuel Masonga aliye kuwa mgombea Ubunge Jimbo la Njombe (Chadema) katika kesi ya kupinga matokeo ya Edwin Swale baada ya kuomba mahakama isiendelee na kesi kabla hajajibiwa na upande unaolalamikiwa.

Mbele ya Jaji Jacob Mwambegele Swale aliomba kujibiwa majibu yake kutoka kwa wakili wa serikali Apmarck Mabruck ambaye alisimama kwa niaba ya msimamizi wa uchaguzi ambaye ni mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Njombe Iluminata Mwenda.

Jaji Mwambegele ameiahirisha kesi hiyo kwa kutoa amri kwa wakili wa serikali kuhakikisha nakala ya majibu inamfikia wakili Swale ndani ya siku nne ili ayapitie majibu hayo na kuanza kusikilizwa kwa kesi hiyo ambayo itatajwa tena.

Walalamikiwa katika kesi hiyo ni pamoja na Mbunge wa jimbo la Njombe kusini Edward Mwalongo, Msimamizi wa uchaguzi ambaye ni mkurugenzi wa mji wa Njombe Iluminata Mwenda na mwanasheria wa mkoa wa Njombe Hilmar Danda ambaye ndyeo alikuwa mratibu wa uchaguzi mkoa wa Njombe.

Kesi hiyo iliyobeba hisia za wakazi wa mji wa Njombe waliofurika mahakamani kujua nini kinaendelea imeahirishwa na Jaji Mwambegele ambapo itasomwa tena Februari 25 mwaka huu.