Friday , 16th Dec , 2016

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi aliyekuwa Mwekahazina wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido, Bw. Issai Mbilu ambaye kwa sasa amehamishiwa Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma na kuagiza arudishwe kujibu tuhuma za ubadhirifu sh. milioni 642.4

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (Kulia), pembeni yake ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha mrisho Gambo

 

“Tunaendelea kudhibiti na kuweka nidhamu ndani ya Serikali. Ukiharibu Longido usitegemee kuhamishiwa wilaya nyingine tunamalizana hapa hapa. Hatuwezi kuhamisha ugonjwa hapa na kuupeleka wilaya nyingine hivyo Mwekahazina huyu arudishwe haraka Longido,” amesisitiza.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido kwenye ukumbi wa Halmashauri hiyo akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Arusha.

Pia amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Bw. Richard Kwitega kumuandikia barua Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) akimuomba amrudishe Mwekahazina huyo katika kituo chake cha kazi cha zamani ili aweze kujibu tuhuma zinazomkabili.

Amesema Serikali haitamvumilia mtumishi wa idara yoyote atakayeharibu jambo halafu kuhamishwa sehemu nyingine, “hivyo naagiza kuanzia sasa nimemsimamisha kazi Mwekahazina huyu na arudi hapa kujibu kwanini ameleta hasara ya hizi fedha. Na nyie watumishi wengine hili liwe funzo kwenu,” amesema.