Monday , 10th Oct , 2016

Tume ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya nchini, imeanza kutumia mbinu mpya za kupambana na kudhibiti usafirishaji na usambazaji wa dawa za kulevya katika maeneo ya mipakani hapa nchini.

Mkuu wa kitengo cha kupambana na kudhibiti dawa za kulevya nchini Kamishna Msaidizi wa Polisi Mihayo Msekela.

Hayo yamebainishwa na mkuu wa kitengo cha kupambana na kudhibiti dawa za kulevya nchini Kamishna Msaidizi, Mihayo Msekhela ambaye amesema mbinu hizo zimeanza kutolewa kwa wakuu wa upepelezi wa jeshi la polisi ngazi za wilaya na mikoa ili kuwabaini wasafarishaji na waingizaji wa dawa hizo.

Kamishna Msekhelea amesema kuwa maeneo ambayo wameanza nayo ni pamoja na mipaka ya Tunduma na Kasumulo iliyopo katika mikoa ya Mbeya na Songwe ambapo biashara hiyo inaonekana kushamiri.

Mkuu huyo wa tume hiyo amesema kuwa maeneo ya mipakani ina changamoto nyingi ikiwemo Ugaidi, wahamiaji haramu lakini kubwa zaidi ni uingizwaji wa madawa ya kulevya ambapo wameanza kutoa mafunzo hayo ili kudhibiti kabisa matukio hayo.