Monday , 31st Dec , 2018

Mbunge wa Jimbo la Chemba Juma Nkamia ameibuka na kutaja vitu anavyojivunia, katika kipindi cha utawala wake kwenye Jimbo hilo kwa kile alichokidai kuwa ametekeleza baadhi ya miradi mikubwa ya maji na ujenzi wa vituo vya afya.

Mbunge wa Jimbo la Chemba Juma Nkamia.

Nkamia ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na www.eatv.tv iliyotaka kufahamu ni kwa namna gani amejiandaa kuelekea mwaka 2019, na kipi ambacho anajivunia kama kiongozi wa wananchi kwenye jimbo lake.

"Kwanza niishukuru serikali kwa kutupatia fedha za kujenga vituo na miradi ya maji, niwaombe tu kwenye zile ahadi ambazo tulizitoa tuhakikishe tunazifikia, kabla ya uchaguzi wa mwaka 2020." amesema Nkamia.

"Ukiniuliza kipi najivunia, ni kuhakikisha tumepata wilaya kamili, tofauti na ilivyokuwa awali, lakini pia najivunia kuwa na miradi mikubwa ya maji, pia wilaya yetu imesimama kwa miguu yake, na pia tumeshapata jengo la Ikulu ndogo." Amesema Nkamia.

Hivi karibuni akizungumza na www.eatv.tv Nkamia alibainisha kuhusu hoja yake ya kutaka uchaguzi mkuu ufanyike baada ya miaka 7 ambapo alisema "msimamo wangu kuhusu miaka 7, uko palepale Mungu akijalia tukiwa hai nitazungumza na chama changu na mamlaka za Bunge kwa mujibu wa taratibu wakiniruhusu nitaupeleka, nilishasema tangu mwanzo''.

''Ila unajua wapingaji wa hoja zangu ni wanaotaka Ubunge haraka na Urais haraka, kiufupi mimi kama unavyonifahamu nikiamua jambo huwa sikwepeshi'', aliongeza.