Thursday , 25th Apr , 2019

Mbunge wa Iringa Mjini, Mch. Peter Msigwa amesema amesikitishwa na kauli ya Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe juu ya juhudi za kuwatafuta watu waliopotea.

Mch. Peter Msigwa

Mbunge wa Iringa Mjini, Mch. Peter Msigwa amesema amesikitishwa na kauli ya Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe juu ya juhudi za kuwatafuta watu waliopotea.

Akichangia katika Bajeti ya Mambo ya Ndani, Mch. Msigwa amesema kwamba jeshi la polisi lenye dhamana ya kulinda raia na mali zake linapaswa kutoa ripoti ya wapi alipo Muandishi wa Habari, Azory Gwanda na si vinginevyo.

Mch. Msigwa amesema kwamba jeshi la Polisi haliwezi kusifiwa kwa matukio kama hayo kwa kuwa uhai wa mtu ni wa thamani na biblia inasema, "mtu mmoja akipotea taifa lazima linung'unike na watu wanaofariki siyo nzi".

Ameendelea kusema kwamba, "polisi imeshindwa kusema nani alimpiga risasi Lissu ambaye anadaiwa kubagaza Taifa, aliyemuua Alphonce Mawazo, Ben Saanane yuko wapi, aliyemnyooshea risasi Nape aliyemteka Roma, lakini hata ripoti ya kutekwa kwa Mohammed Dewji mpaka leo haijatoka".

Akikazia katika suala hilo, Msigwa amesema kazi ya Polisi ni kulinda raia na mali zao, na kwamba IGP aliahidi kulitolea ufafanuzi suala la utekwaji wa mfanyabiashara huyo baada ya Rais kusema watanzania siyo wajinga lakini mpaka sasa hakuna kilichoendelea.

"Polisi ana wajibu wa kusema kwanini raia wanauawa kwa kuwa wao ndiyo wenye mabomu  na kila kitendea kazi. kazi yao ni kutulinda na siyo tukae tuseme oooh wanang'atwa na mbu sasa kwani wana kazi gani?", amesema Msigwa.

Mbali na hayo Mch. Msigwa amesema kwamba jeshi hilo la polisi limekuwa likiwatengenezea raia kesi na mbaya zaidi huko kwenye vituo vya polisi na bado wanawafanyia unyanyasaji huku akibainisha kwamba hata yeye ameshwahi kuwa muhanga wa kutengenezewa kesi.

Akiongezea amesema kwamba hawezi kujadili kwamba polisi wanang'atwa na mbu kwa kuwa hiyo ni kazi yao kwa kuwa wanalipwa na wala siyo kwamba wanawafanyia huruma wananchi.