Wednesday , 14th Dec , 2016

Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha leo imemwachia huru  aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana Mkoa wa Arusha (UVCCM), Lengai ole Sabaya katika kesi ya  kujifanya mtumishi wa umma idara ya usalama wa Taifa (TISS).

Lengai ole Sabaya

 

Hatua hiyo imekuja baada ya upande wa mawakili wa serikali kuiomba  Mahakama hiyo mbele ya hakimu Gwantwa Mwankuga  kufuta kesi hiyo, kutokana na Jamuhuri kutokuwa na lengo la kuendelea na kesi hiyo.

Kabla ya kufutwa kesi hiyo  leo wakili wa serikali Grace Madikenga alidai mahakamani hapo kuwa upande wa serikali hauna lengo la kuendelea na kesi hiyo hivyo waliiomba mahakama hiyo kuifuta kesi hiyo.

Kesi hiyo leo ilitarajiwa kusikilizwa ambapo shahidi wa kwanza wa upande wa serikali,Inspekta Rogathe alitarajiwa kutoa ushahidi wake.

AKAMATWA TENA

Baada ya mahakama hiyo kumuachia huru Sabaya, Jeshi la polisi lilimkamata tena nje ya viwanja vya mahakama hiyo na kumpeleka katika kituo kikuu cha polisi.

Sabaya amekamatwa majira ya saa nne, asubuhi ambapo aliondolewa mahakamani hapo na gari la polisi lililokuwa na namba za usajili T. 953 CSZ.

Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Arusha, Charles Mkumbo amesema Sabaya amekamatwa  kwa kesi hiyo hiyo na kuwa wanafanya taratibu na watakapomaliza atafikishwa tena mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.