Tume ya taifa ya uchaguzi imeombwa kufikiria kuongeza muda zaidi wa uandikishaji katika daftari la kudumu la wapiga kura wilayani Bunda mkoani Mara baada ya kuibuka kwa changamoto nyingi katika zoezi hilo likiwemo tatizo kubwa la kuharibika mara kwa mara kwa mashine hizo za mfumo wa BVR.
Mbunge wa viti maalum mkoa wa Mara Esther Bulaya, ametoa wito huo baada ya kujiandikisha na kutembelea vituo kadhaa vya uandikishaji mjini Bunda, ambapo amesema tatizo la kuharibika kwa mashine hizo za BVR kunaweza kusababisha idadi kubwa ya wananchi kukosa fursa ya kundikishwa katika zoezi hilo muhimu.
"Nimetembelea vituo mbalimbali, tatizo kubwa ni idadi ndogo ya watu wanaoandikishwa kwa siku, kwa mfano sabasaba wanatakiwa kuandikishwa watu 1000 lakini hadi sasa wameandikisha 200 pekee..... Nitakwenda kuwaambia Tume waongeze muda wa kuandikisha"
Hata hivyo Bulaya amesema uchache wa vifaa katika zoezi hilo la uandikishaji ni moja ya changamoto kubwa ambayo imebainika katika maeneo mengi wilayani humo.