Monday , 5th Sep , 2016

Jeshi la polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limesema limewakamata majambazi 14 na wengine 3 kufariki dunia katika mapambano baina ya jeshi la polisi na majambazi katika siku za hivi karibuni kwenye eneo la Vikindu mkoani Pwani.

Kamishna Simon Sirro, akionesha mbele ya waandishi wa habari, silaha zilizokamatwa

Akitoa taarifa ya operesheni tofauti tofauti zilizofanywa na jeshi la hilo katika kusambaratisha makundi ya majambazi ambao wameshiriki kufanya matukio mbalimbali ya uhalifu nchini, Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam CP Simon Sirro amesema mbali na majambazi hao wamekamata pia bunduki 23 risasi 835, Bullet Proof 3, Sare za Polisi, Pingu 48 na Radio Call 12 zilizokuwa zikitumiwa na majambazi hao.

Aidha CP Sirro amesema katika mapambano hayo na majambazi jeshi hilo limempoteza askari polisi mmoja na kueleza kuwa miongoni mwa majambazi hao hakuwepo askari mstaafu kama ilivyodaiwa, bali walikamata sare feki zilizokuwa zikivaliwa na majambazi hao katika matukio ya uhalifu, sambamba na kuwataka wanajamii kuendelea kushirikiana na jeshi hilo katika kuwafichua wahalifu.