Saturday , 23rd Jan , 2016

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha alitangaza kufuta matokeo ya Uchaguzi Zanzibar, uliofanyika Oktoba 25, 2015 tarehe ya 28,10,2015.

Jecha alisema kuwa, ZEC ilifuta matokeo ya uchaguzi kutokana na kukiukwa kwa sheria na taratibu mbalimbali za uchaguzi wakati wa utekelezaji wa zoezi hilo na kusisitiza kuwa uchaguzi ungerudiwa ndani ya siku 90.

Hizi ndizo sababu nane zilizotolewa na mwenyekiti wa tume ya uchaguzi wa kisiwani Zanzibar Bw Jecha Salim Jecha kuhusu kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi.

1. Makamishna wa uchaguzi katika tume hiyo walipigana kutokana na tofauti zao za kisiasa.

2. Makamishna walikuwa na upendeleo fulani.

3. Katika vituo vyengine, hususan kisiwani Pemba, kura zilizopigwa zilikuwa zaidi ya zilizosajiliwa.

4. Masanduku ya kupigia kura hayakupewa ulinzi wa kutosha na mawakala pamoja na maafisa wa uchaguzi.

5. Mawakala wa vyama walifukuzwa katika vituo kadhaa.

6. Vijana walivamia vituo vya kupigia kura wakiwa na lengo la kuzua ghasia.

7. Vyama vya kisiasa vimekuwa vikiingilia tume hiyo.

8. Kura ziliharibiwa hususan zile kutoka Pemba.

Aidha uchaguzi wa Zanzibar utarudiwa siku ya Jumapili tarehe 20 mwezi wa Machi, 2016 ambapo wagombea walewale ndio watakaopigiwa kura na hakuna marudio ya kampeni.