Friday , 18th Jul , 2014

Serikali ya Tanzania imesaini makubaliano na serikali ya Kenya kwa ajili ya kuanza kuwauzia nafaka aina ya mahindi, ili kukabiliana na upungufu wa chakula unaoikabili nchi hiyo.

Akizungumza jijini Arusha wakati wa kusaini makubaliano hayo ambayo yalihudhuriwa na Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilomo, Chakula na Ushirika nchini Tanzania Bi. Sophia Kaduma, amesema serikali ya Kenya waliandika barua kuja nchini wakiomba msaada wa chakula.

Bi. Sophia amesema endapo wafanyabiashara watapeleka mahindi Kenya kuanzia sasa, tani moja itauzwa kwa fedha ya Kenya shilingi 32,777 na kwa upande wa Tanzania yatauzwa shilingi 523,461 kwa tani moja.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo wa nchini Kenya kutoka, Sicily Kariuki amesema wameshukuru kwa ushirikiano mzuri wa nchi hizo mbili na kushukuru kwa kuwepo Jumuiya ya Afrika Mshariki, kwani amesema imewezesha tatizo lao kutatulika kwa haraka.

Wakati huo huo, serikali jana imetiliana saini ya makubaliano na serikali ya watu wa Korea ambapo chini ya makubaliano hayo Tanzania sasa itaweza kupata misaada ikiwemo ya fedha ambayo itaelekezwa katika maeneo mbali mbali ikiwemo sekta ya Kilimo na Maji.

Katika makubaliano hayo serikali ya Tanzania iliwakilishwa na Katibu mkuu wa wizara ya Fedha na Uchumi Dkt. Servacius Likwelile na kwa upande wa serikali ya watu wa Korea imewakilishwa na Balozi wa Korea nchini Bw. Chung IL.

Akizungumza katika hafla hiyo Katibu mkuu wa Hazina Dk. Servacius Likwelile amesema sekta nyingine zitakazonufaika na misaada hiyo ni pamoja na kuboresha mifumo ya maji ambapo kwa kuanzia mwaka ujao Tanzania itapata zaidi ya dola za marekani milioni 10 kama msaada na dola za Marekani zaidi ya milioni 100 kama mkopo ambazo zitaelekeza kwenye ujenzi wa miradi ya barabara.