Tuesday , 4th Apr , 2017

Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) imekusanya mapato ya jumla ya shilingi za Tanzania trilioni 10.87 katika kipindi cha miezi tisa ya mwaka wa fedha ambao unaoishia Juni mwaka huu, huku kukiwa na dalili za kufikia lengo la makusanyo iliyojiwekea.

Richard Kayombo - Mkurugenzi wa Elimu na Huduma kwa Mlipakodi wa TRA

Akizungumza na wanahabari leo Jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa Elimu na Huduma kwa Mlipakodi wa TRA Bw. Richard Kayombo amesema kiwango hicho ni sawa na ukuaji wa asilimia 9.99 wa makusanyo ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita.

Aidha, Bw. Kayombo amesema bado mwelekeo wa makusanyo ya mapato ni mzuri kutokana na mwitikio wa wananchi katika kulipa kodi kwani takwimu za makusanyo ya mwezi Machi zinaonesha kuwa TRA imekusanya shilingi trilioni 1.34 ikiwa ni sawa na ukuaji wa asilimia 2.23.