Thursday , 13th Oct , 2016

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema iliamua kurejesha fedha zilizobaki baada ya zoezi la uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kiasi cha bilioni 12 ili kuiunga mkono serikali katika nia yake ya ya kupunguza matumizi yasiyo ya lazima kwa ajili ya maendeleo

Ramadhan Kailima - Mkurugenzi wa Uchaguzi NEC

Akizungumza Jijini Dar es salaam katika kipindi cha HOTMIX kinachorushwa na EATV, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Uchaguzi Kailima Ramadhani amesema, tume ilifanya hivyo kwa nia njema ingawa wananchi ingawa wananchi walionesha kushangazwa na kitendo hicho, ikizingatiwa kuwa tume hiyo ilikuwa ikilalamika kutokuwa na fedha za kutosha.

Kwa mujibu wa Kailima, katika mwaka wa fedha 2013/14, fedha kwa ajili ya tume hiyo hazikutosha na ndiyo maana kukawa na taarifa za tume hiyo kukumbwa na upungufu wa kibajeti hali iliyosababisha tume hiyo kutotimiza kikamilifu jukumu la elimu kwa mpiga kura pamoja na suala la kuboresha daftari, lakini katika mwaka wa fedha uliofuata (2014/15) bajeti iliyotengwa kwa ajili ya uchaguzi mkuu, ilitosha na kufanikisha shughuli nzima ya uchaguzi, na hatimaye kiasi hicho cha fedha kubaki.

“Wananchi wanatakiwa wafahamu kwamba fedha tulizorejesha zilibaki kutokana na fedha tulizopewa kwa mwaka wa fedha 2014/2015 ambapo ndizo zilibaki baada ya zoezi la uchaguzi mkuu kumalizika ndiyo maana tukarejesha ambapo kwa kipindi cha sasa tusingefanya hivyo tungeweza kutumbuliwa” Amesema Kailima

Aidha Kailima amesema Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa sasa imejipanga vizuri na imeanza zoezi la kutoa elimu ya upigaji kura mapema ili kuondoa malalamiko kwa wananchi na kuwaweka tayari kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa pamoja na uchaguzi mkuu mwaka 2020.