Friday , 25th Mar , 2016

Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Dar es salaam Salma Mwasa (CUF) amesema fedha zilizokuwa zikitengwa asilimia 10% kwa ajili ya kinamama na vijana kuwasaidia katika huduma za kijamii na mikopo midogomidogo katika halmashauri zilikuwa hazifiki walengwa.

Mwasa ameyasema hayo alipokuwa akizungumza katika kipindi cha SupaMix kinachorushwa na East Africa Radio siku ya Jumatatu hadi Ijumaa na kusisitiza kuwa fedha hizo zingekuwa zinatoka kama ilivyopangwa huduma za zahanati nyingi nchini hali isingekuwa mbaya kama ilivyo sasa.

''Kilichokuwa kinasababisha kukwama kwa miradi pamoja na hospitali nyingi kukosa vifaa katika halmashauri zetu ni utawala uliokuwepo hivyo sisi kwa hapa Dar es salaam tutaonyesha mfano wa uwajibikaji katika kusimamia fedha ziweze kutoka kwa wakati na kwenda kwenye maeneo husika''-Amesema Salma Mwasha.

Mwasha amesema katika kuhakikisha kwamba mchango wake unakuwa wa manufaa katika jamii amekusudia kuhakikisha anatoa vifaa vya afya kwa kina mama katika hospitali 50 kupitia Foundation yake inayojulikana kama Salma Mwasa Foundation kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo nchini.

Mwasa pia amebainisha kwamba wanawake wabunge wa viti maalum Bungeni wana mchango mkubwa katika kuhakikisha huduma za kijamii hasa kwa wanawake zinapatikana kwa wakati nchini kwa kuweka itikadi za vyama vyao pembeni na kuwatetea wanawake na watoto kupata haki zao za msingi.