Tuesday , 11th Oct , 2016

Makamu wa Rais wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amekiri kuwa kuna changamoto ndogo ya upatikanaji wa madawa nchini kwa sasa.

Makamu wa Rais wa Tanzania, Mh. Samia Suluhu Hassan

Mhe. Samia ametoa kauli hiyo leo Jijini Dar es Salaam wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la wazazi katika Hospital ya Mwananyamala, jengo linalojengwa kwa ufadhili wa Amsons Group of Companies.

Mhe. Suluhu ametoa kauli hiyo ikiwa imepita siku moja tu tangu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu kusema hakuna uhaba wa dawa nchini.

Mhe. Suluhu amesema hiyo ni changamoto ya muda tu ambayo tayari serikali imechukua hatua za haraka kuhakikisha hakutokei tena upungufu wa madawa.

Aidha Mhe. Samia amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Bw. Paul Makonda kutafuta magari mawili yakubeba wagonjwa katika Hospital ya Mwananyamala ndani ya miezi mitatu na kuhakikisha Hospital hiyo inaweka mpango mikakati mzuri wa matumizi ya fedha zake inazopata ili kusaidia serikali kutatua changamoto zake.

Kwa upande wake Mganga Mfadhiwa wa Hospitali ya Mwananyamala Dkt. Daniel Nkungu ameiomba serikali kulipa madeni ya watumishi wanaoidai serikali kwa kipindi cha miaka mitatu na kutatua ukosefu wavifaa tiba.

Kwa upande wake waziri wa nchi, ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora Mhe. Angela Kairuki ameahidi kufanyia kazi tatizo la malipo ya watumishi na uhaba wa watumishi katika hospitali hiyo.