Monday , 10th Mar , 2014

Serikali ya Tanzania imetoa agizo kuhakikisha uvutaji wa sigara sehemu za uma unazuiwa ili kulinda afya za watu wasiovuta sigara.

Halmashauri na serikali za mitaa nchini Tanzania zimetakiwa kuhakikisha zinasimamia na kutekeleza kwa vitendo sheria inayokataza uvutaji sigara katika maeneo ya wazi na yale yenye mikusanyiko mikubwa ya watu, ili kuepuka madhara ya kiafya yanayoweza kuwapata watu wasiovuta sigara.

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Seif Rashid, ametoa agizo hilo leo jijini Dar es Salaam wakati akizungumzia maadhimisho ya siku ya afya ya figo, ambapo ametaja moja ya sababu zinazochangia ugonjwa huo kuwa ni uvutaji sigara na matumizi ya tumbaku.

Kwa mujibu wa Dkt Rashid, sigara ina madhara mengi kwa afya ya binadamu, na kwamba kiwango cha watu wenye matatizo ya figo kinaweza kupungua iwapo serikali za mitaa zitatekeleza ipasavyo sheria inayokataza uvutaji wa sigara katika halaiki ya watu.