Monday , 7th Nov , 2016

Takribani vijana milioni tano nchini Tanzania, hawana shughuli inayoeleweka ya kuwaingizia kipato sambamba na elimu ya ujasiriamali utakaowawezesha kujiajiri.

Beng'i Issa

Hali hiyo imelilazimu Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kuja na mipango kadhaa kwa ajili ya kuinua uchumi wa kundi hili katika jamii.

Katibu Mtendaji wa Baraza hilo Bi. Beng'i Mazana Issa amesema hayo leo wakati wa tathmini ya mradi wa Kijana Jiajiri, ulioanza kutekelezwa katika baadhi ya mikoa nchini kwa lengo la kuona ni jinsi gani mradi huo utakuwa suluhisho la uchumi pale utakapotekelezwa kwa vijana katika mikoa yote nchini.

Mradi wa Kijana Jiajiri unatekelezwa na taasisi ya TECC chini ya uratibu wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) huku Mratibu wa Mradi huo Bw. Sosthenes Sambua akieleza changamoto wanazokutana nazo wakati wa kutekeleza mradi huo kuwa ni mabenki na taasisi za kifedha kutokuwa tayari kutoa mikopo kwa vijana waliopatiwa mafunzo kutoka mradi wa Kijana Jiajiri