Tuesday , 21st Jul , 2015

Waandishi wa habari nchini wametakiwa kuwa na ujasiri katika kufanya kazi zao hasa katika kuandika habari za uchaguzi, ili kupata habari sahihi zisizokuwa na upendeleo kwa masilahi ya wanasiasa.

Mshauri wa masuala ya habari na mawasiliano wa shirika Utangazaji la Uingereza (BBC), Ndimara Tegambwage.

Wito huo umetolewa jana mkoani Mtwara na mshauri wa masuala ya habari na mawasiliano wa shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Ndimara Tegambwage katika semina kwa waandishi wa habari kuhusu namna ya kuandika habari za uchaguzi.

Amesema lengo la kutoa semina hiyo ni kuwawezesha waandishi wa habari kuelewa nafasi ya taaluma yao katika kuandika habari katika kipindi hiki ambacho taifa linaelekea katika uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na Rais.

Aidha Tegambwage ameongeza kuwa waandishi wa habari wanatakiwa kupewa kila taarifa na tume kuhusu mambo yanayohusiana na uchaguzi ili waweze kuwataarifu wananchi jinsi hali ya uchaguzi inavyokwenda.

Ameongeza kuwa waandishi wengi siku hizi wanaandika habari kwa kufuata matakwa ya chama fulani na kufanya taaluma ya habari kuonekana nayo inakuwa na harakati za kisiasa.