Sunday , 16th Oct , 2016

Serikali imesema kipaumbele chake cha kuboresha elimu imeanza kutekeleza kwa kuanza kutoa elimu ambayo inatoa wahitimu wenye ujuzi na maarifa kulingana na ngazi wanazohitimu.

Prof. Joyce Ndalichako, Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako wakati akizungumza na wadau wa elimu nchini, ambao wamekutana kwa lengo la kujadili njia sahihi za kufuatwa, ambazo zitasaidia elimu ya Tanzania kuwa ya ushindani na nchi zingine.

Amesema katika kuhakikisha lengo la kuboresha elimu linafikiwa kwa asilimia zote, lazima wasimamizi wajiwekee mikakati ya kufikia malengo kwa wakati

Katika suala la elimu ambayo iko nje ya mfumo rasmi ambapo takribani watoto milioni mbili ambao wanapaswa kuwa shuleni lakini hawako shuleni, amewaagiza wakuu na wasimamizi wa elimu nchini kuweka mifumo endelevu ya kusimamia ili kila mara kusiwe na ulazima wa kuanzisha mipango mipya kwakuwa elimu ni haki ya msingi kwa kila mtu kuipata.

Waziri Ndalichako amesema wadau wa maendeleo nao waangalie tatizo ni nini linalofanya elimu ya Tanzania kuendelea kuwa na changamoto, na wawasilishe katika ofisi yake tayari kwa kuanza kulitatua.