.jpg?itok=xmXK_ZFp×tamp=1473564741)
Kibatala alidai hayo mbele ya Hakimu Mkuu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam Cyprian Mkeha, baada ya Wakili wa Serikali Mwandamizi Shedrack Kimaro kuiomba Mahakama isimame kusikiliza kesi ya msingi kwa sababu wameshawasilisha kusudio la kukata rufaa.
Wakili huyo alipinga kusimama kusikilizwa kwa kesi hiyo kwa sababu mara ya mwisho mahakama ilielekeza kuwa upande huo unatakiwa kuleta mashahidi, lakini hivi sasa wanachokifanya ni kukimbilia mahakama kuu kuzuia kesi zisisikilizwe.
"Imekuwa kama mchezo wa Jamhuri kukimbilia Mahakama Kuu ili kesi zisiendelee kusikilizwa sasa kama wao wameshindwa kuleta mashahidi basi mahakama imuachie mteja wangu kwa kifungu cha 225," alidai Kibatala.
Awali, Kimaro alitoa ombi hilo kwa sababu wamewasilisha kusudio la kukata rufaa kupinga uamuzi wa mahakama hiyo kukataa kupokea CD ambayo inaonesha askofu huyo akimtolea lugha hiyo Askofu Pengo.
Pia mahakama ilikata kupokea kama kielelezo katika kesi hiyo ripoti ya mtaalamu wa CD, picha zenyewe na barua iliyoandikwa kuwa vielelezo vilitoka kwa ZDCO kwenda kwa mtaalamu wa picha.
Kimaro alidai kwa sababu ya masuala hayo ndiyo maana hakuleta mashahidi, kwa hiyo kwa sababu wameshaanza utaratibu wa kushughulikia rufaa, lazima kesi ya msingi isimame.
Hakimu Mkeha alisikiliza hoja hizo, ambapo Juni 2 mwaka huu ndiyo atapanga tarehe ya kutoa uamuzi kama kesi hiyo inasimama au la.
Katika kesi hiyo, Gwajima anadaiwa kuwa kati ya Machi 16 na 25, 2015 Tanganyika Packers Kawe alitumia lugha chafu na kumdhihaki Muhadhama wa Kanisa Katoliki Askofu Kardinal Polcarp Pengo.