Tuesday , 26th Apr , 2016

Tanzania leo imeadhimisha miaka 52 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar bila maadhimisho rasmi.

Tanzania leo imeadhimisha miaka 52 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar bila maadhimisho rasmi baada ya Rais wa Jamuhuri ya muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli kuzielekeza fedha zilizotengwa kwa ajili ya maadhimisho hayo kuzipeleka kujenga barabara ya Uwanja wa Ndege hadi Ghana jijini Mwanza.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli aliagiza fedha shilingi bilioni 2 zilizotengwa na serikali kwa ajili ya sherehe za Muungano zielekezwe katika ujenzi wa barabara ya Airport hadi Ghana jijini Mwanza zitumike katika ujenzi huo uliokusudiwa na serikali ya awamu ya tano.

Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Utumishi na Utawala Bora, Selemani Jaffo akiongea na East Africa Television amewatoa hofu Watanzania bara na visiswani kuwa pesa hizo zitafanya kazi kwa ajili ya pande zote mbili bila kubagua kwakuwa Rais Magufuli anania njema na taifa hili.

Amesema serikali ya awamu ya tano haitaki kufanya kazi kwa matabaka na imejihakikishia kusimamia malengo ya muungano yaliyowekwa na waasisi maraisi wa kwanza wa Tanzania Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Rais wa kwanza wa Zanzibar Hayati Abed Amani Karume ulioundwa mwaka 1964.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Kazi,Vijana na Ajira,Mhe Anthony Mavunde amesema hatua ya Rais kuamua kubana matumizi ya fedha za sherehe ya Muungano na kupeleka pesa hizo kwa ajili ya huduma za kijamii nikitendo ambacho kitasaidia watanzania wote kupata huduma muhimu kuliko pesa hizo zingeenda kwa watu wachache.