Tuesday , 22nd Aug , 2017

Wanaume wanne wamefikishwa kwenye mahakama ya Afrika Kusini kujibu mashtaka ya ulaji nyama ya binadamu, baada ya madai kuwa mmoja wao alifika katika kituo cha polisi na kusema kuwa amechoka maisha ya kula nyama ya binadamu.

Taarifa zinasema kuwa  baada ya kujisalimisha na kufanyiwa mahojiano mwanaume huyo alionyesha sehemu ya mguu na mkono wa binadamu na baadaye polisi wa nchi hiyo kuandamana naye hadi nyumba moja iliyo mtaa wa KwaZulu-Natal, ambapo  miili zaidi ya binadamu ilipatikana.

Kati ya wanaume hao waliokamatwa, wawili wanadaiwa kuwa ni waganga wa kienyeji wanashtakiwa kwa mauaji au kupanga kuua walifikishwa katika mahakama ya Estcourt kilomita 175 kaskazini magharibi mwa mji wa Durban.

Nyumba hii ni mahali nyama hizo zilipokutwa 

Kupitia  Shirika la Utangazaji la Uingereza la (BBC)  Msemaji wa polisi amesema  kuwa kuna uwezekano kuwa wanaume hao wanne walio na umri wa kati ya miaka 22 na 32 ni sehemu ya genge kubwa la wahusika wa matukio hao.

Pamoja na hayo Uchunguzi wa tukio hilo bado unaendelea na polisi wamewashauri watu ambao ndugu na jamaa zao wametoweka kujitokeza.

Wachunguzi wa matukio ya uhalifu wameitwa kutambua sehemu hizo za binadamu, kwa kuwa haijulikani kama sehemu hizo ni za mwili wa  mtu mmoja au watu wengi.