Friday , 16th Dec , 2016

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaagiza wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya ya Longido mkoani Arusha kufanya msako wa nyumba hadi nyumba na kuwakamata wote watakaokutwa wanafanya biashara ya dawa za kulevya.

Dawa za kulevya aina ya mirungi

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido kwenye ukumbi wa Halmashauri hiyo akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Arusha.

“Wilaya hii ina sifa mbaya ya kuwa kitovu cha kusafirisha dawa ya kulevya zikiwemo  bangi na mirungi. Hivyo nawaagiza wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama waendeshe msako kwa kila nyumba na atakayekamatwa achukuliwe hatua. Dawa za kulevya zinadhohofisha nguvu kazi ya Taifa,”.

“Ukivuta bangi unapishana na kauli mbiu ya Hapa Kazi Tu kwani unakwenda kulala jambo ambalo hatuwezi kulikubali. Watakaokutwa wanauza au kununua mirungi na bangi wakamatwe na kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwa pamoja na kutaifisha magari yanayotumika kubeba bidhaa hiyo haramu,” amesema.