Wednesday , 31st Dec , 2014

Aliyekuwa  mwanasheria mkuu wa  serikali  Jaji Fredrick Werema amepokelewa  kijijini kwake  baada  ya  kujiuzulu  nafasi  hiyo  hivi  karibuni.

Jaji Fredrick Werema baada ya kuwasili kijijini kwake

Jaji Werema amepokelewa  kijijini kwake  baada  ya  kujiuzulu  nafasi  hiyo  hivi  karibuni  huku  wananchi   wa  kijiji  hicho  wakiwataka  watuhumiwa  wote katika sakata  la  akaunti   ya  Tegeta Escrow kujiuzulu nafasi  zao  ili  kulinusuru taifa  kuingia katika mgawanyiko  na machafuko  ambayo wamedai  yanaweza  kuhatarisha  amani.
 
Wakizungumza baada   ya  kumpokea  Jaji   Werema  muda  mfupi   baada  ya kuwasili  katika  kijiji   hicho cha Kongoto   tarafa   ya  Kiagata  mkoani  Mara, wananchi  hao  wamempongeza  kiongozi huyo  kwa   kuchukua  hatua  ya  kujiuzulu  nafasi   hiyo   ya uanasheria  mkuu  wa  serikali.

Wananchi hao pia wamesema  ni  jambo  la  busara  kwa  kiongozi  wa  umma  kuchukua  uamuzi  kama  huo  katika  kulinusuru  taifa  lake hasa  baada  ya  kutuhumiwa  katika   sakata  hilo.
 
Kwa  upande  wake  Jaji  Fredirick  werema, akizungumza  na   wananchi  hao amesema hawezi kuteteleka kwa  uamuzi  wake   wa  kujiuzulu  huku   akisema  ni  jambo  la  busara   kama  kiongozi  wa umma  unapohusishwa  na   tuhuma  zozote kukubali  kwa  hiari  yako  kuwajibika  ili  kulinda  maslahi   ya  taifa.
 
Kuhusu  chama cha demokrasia kushinda  katika  kijiji  chake  kwa  nafasi  ya uenyekiti wakihusisha ni kutokana  na  sakata  la  Escrow,  Jaji  Werema amesema hatua hiyo imetokana  na  wananchi kuchoshwa  na baadhi  ya  viongozi  wa  CCM  katika  eneo hilo hivyo  kuomba  wananchi  kumpa kiongozi huyo  ushirikiano katika  kutimiza wajibu wake.