Tuesday , 4th Apr , 2017

Mwanaharakati wa masuala ya jinsia nchini Tanzania Dkt. Avemaria Semakafu amemshukuru Rais Magufuli kwa kumteua kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu huku akiahidi ushirikiano na watendaji wengine wa wizara katika kusukuma ajenda ya elimu nchini.

Dkt. Semakafu katika moja ya harakati zake za kutoa mafunzo kwa wanawake

Akizungumza na EATV kwa njia ya simu mara baada ya uteuzi huo kutangazwa, Semakafu ambaye pia ni Mhadhiri Chuo Kikuu cha Tiba na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) ameahidi kuitumikia nafasi hiyo kwa uaminifu na uadilifu mkubwa.

Kuhusu kuendeleza harakati zake, amesema ni vigumu kuzifanya harakati za jinsia lakini atajitahidi kutumia uwezo wake kusukuma masuala kadhaa yahusuyo elimu kwa mtoto wa kike kwa ushirikiano na watu atakaowakuta wizarani, lakini pia kwa kufuata miongozo iliyopo.

"Kwenda wizara ya elimu ni fursa kwangu lakini ifahamike kuwa nakwenda mahali ambapo tayari kuna mipango ambayo tayari imeshawekwa, kwahiyo ni kwenda kuangalia changamoto ambazo zimeanishwa na mipango iliyowekwa  na jinsi gani itatekelezeka katika kushughulikia kuzitatua... Nitakwenda kujifunza na kwa kutumia harakati zangu, waliopo pale pia watajifunza kwangu" Amesema Semakafu

Dkt. Semakafu anafahamika zaidi nchini kwa kutoa na kuchangia mada mbalimbali kupitia mihadhara na vipindi vya luninga vinavyohusu mijadala mbalimbali ya kijamii na kitaifa. Pia alikuwa ni mjumbe katika Bunge Maalum la Katiba mwaka 2014, wakati huo akiwa mratibu wa Mtandao wa wanawake na Katiba (Ulingo) 

Msikilize hapa..