Thursday , 18th Aug , 2016

Baraza la Sanaa Tanzani (BASATA) limewataka washiriki wa Dance100% ambao wamefanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali kujisajili katika baraza hilo ili kazi zao ziweze kutambulika kisheria.

Afisa Msajili wa Sanaa wa BASATA Agustino Makame alipokuwa akizungumza na washiriki wa shindano la Dance100% juu ya umuhimu wa kujisajili Jijini Dar es salaam.

Hayo yameelezwa hii leo Jijini Dar es salaam na Afisa Sanaa wa BASATA Agustino Makame, wakati wa semina kwa makundi yaliyofuzu hatua ya nusu fainali ya Dance100% ambapo ameeleza faida mbalimbali za wasanii kujisajili katika baraza hilo.

“BASATA ndiyo chombo ambacho kipo kisheria nchini kwa ajili ya kusajili na kusimamia tasnia ya sanaa nchini kwa hiyo umuhimu wa kujisajili ni pamoja na kutambulika kazi zao kisheria hata ikitokea wizi wa kazi msanii anaweza kuja BASATA na akatambulika pia inapotokea msanii anataka kufanya shughuli ambayo inahitaji kibali atatambulika kirahisi” Amesema Bwana. Makame.

Makame ameongeza kuwa hata kama msanii anataka kwenda kufanya kazi ya sanaa nje ya nchi atashughulikiwa kirahisi katika balozi zetu kwa kuwa anatambulika na BASATA.

Aidha kwa upande wake Mkuu wa Matukio ya Sanaa kutoka BASATA Bwana. Kurwijira N Maregesi amesema nidhamu ni kitu muhimu katika kazi yoyote halali hivyo wasanii hao wanatakiwa kuwa wabunifu na pia kuwa na nidhamu ya hali ya juu ili waweze kupokelewa vyema na jamii.

Kwa upande wake Mratibu wa Shindano la Dance100% kutoka EATV Bhoke Egna amewaahidi washiriki wa shindano hilo kuwa kazi yoyote ya burudani itakayoandaliwa na EATV watapewa kipaumbele cha kuburudisha watu kupitia sanaa yao ili wazidi kutambulika na jamii.

Pamoja na hayo mmoja wa majaji wa shindano hilo Lotus amewataka washiriki kuzingatia suala la sare wakati wa shindano pamoja na kutotafuna vitu wakati wakiwa jukwaani kwani kwa kufanya hivyo kutawapunguzia alama.

Shindano la Dance100% linaendeshwa na EATV kwa udhamini maridhawa wa VODACOM na COCA-COLA na kuoneshwa na EATV pekee kila Jumapili kuanzia saa moja kamili jioni.

Tags: