Tuesday , 16th Aug , 2016

Shindano la Dance100% ambalo limemaliza hatua ya robo fainali wiki iliyopita na kuyapa makundi 10 nafasi ya kujiandaa katika hatua ya nusu fainali lina binti mmoja pekee ambaye anashiriki shindano hilo.

Kibibi Ramadhani binti pekee aliyefuzu hatua ya nusu fainali shindano la Dance100%

Kibibi Ramadhani ndiye binti pekee ambaye amesalia katika shindano la Dance100% akiwa katika kundi la DDI ambalo linafanya shughuli zake katika eneo la Mango Garden Kinondoni Jijini Dar es salaam.

Akizungumza na EATV Kibibi amesema anaipenda sana sanaa ya kucheza na ni kipaji ambacho amekuwa nacho tokea utotoni hivyo kupitia Dance100% anaamini atafahamika zaidi katika maeneo mbalimbali na kuweza kupanda ngazi moja kwenda nchini nyingine kwa kuwa uwezo alionao ni mkubwa sana.

“Napenda Dance sana mwaka 2007 nilijiunga na kundi moja linaitwa Gombezi ambapo niliweza kujifunza mambo mengi kuhusu namna ya kuweza kutawala jukwaa na kufanya kazi na makundi kwa kuchanganyika na wanaume kwa kuwa wasichana wengi wanaogopa” Amesema Kibibi

Kibibi ameongeza kuwa lengo lake ni siku moja awe ‘dancer’ mkubwa Tanzania kwa kuwa upande wa kike wanaohusika na sanaa hiyo bado ni wachache hivyo anaamini akiongeza juhudi atafika mbali zaidi.

Kwa upande wake mmoja wa washiriki wa kundi hilo Samson Morisi amesema binti huyo anafanya vizuri sana kiasi kwamba kundi lao linatamani mabiti wengine wangejitokeza ila wengi ni waoga na mazoezi makali hivyo wengi wanaojaribu huishi kukwama tofauti na Kibibi.

Shindano la Dance100% linaendeshwa na EATV kwa udhamini maridadi wa Vodacom na Coca-Cola, na kuoneshwa kupitia EATV pekee kila Jumapili saa moja jioni.

Kundi la DDI ambalo Kibibi ni ni mmoja wa wanaoliunda walipokuwa wakionyesha ufundi hatua ya robo fainali
Tags: