Wednesday , 22nd Aug , 2018

Msanii mkongwe wa filamu bongo, Vincent Kigosi maarufu kama 'Ray' amefunguka na kumwagia mijisifa muigizaji Salim Ahmed 'Gabo Zigamba', kuwa ni miongoni mwa wanaume wanaofanya vizuri katika uigizaji nchini Tanzania.

Vincent Kigosi akiwa katika picha ya pamoja na Gabo Zigamba.

Ray ametoa pongezi hizo wakati alipokuwa anapiga stori na www.eatv.tv na kusema kila muigizaji mpya anayeingia katika ulingo wa sanaa, huwa anakuwa na ubora wake kulingana na nyakati alizozikuta. 

"Gabo ni msanii mzuri siwezi kukataa jambo hilo na ni kijana wangu ambaye anafanya kazi nzuri sana na tunaheshimiana mimi na yeye, lakini siwezi kusema mengi kuhusu yeye juu ya watu wanavyomzungumzia. Kila kitu kina wakati wake na inapokuja 'brand' mpya au muigizaji mpya na kitu cha utofauti lazima watu wamkubali huyo hilo halipingiki popote pale", amesema Ray.

Gabo ni miongoni mwa wasanii walioweza kupata mafanikio makubwa katika sanaa ya filamu nchini Tanzania, kwa kujizolea tuzo mbalimbali za uigizaji hadi hivi sasa.

Mwaka 2016, Gabo alikuwa miongoni mwa wasanii walioshiriki katika kuwania tuzo za 'EATV AWARDS' na kufanikiwa kuondoka na tuzo mbili, ikiwemo ya uigizaji bora wa kiume pamoja na filamu bora ya mwaka 'safari ya gwalu'.