Monday , 20th Aug , 2018

Imeelezwa kuwa katika masuala ya Ndoa hayana muda sahihi wala kanuni inayoongoza mioyo katika uanzishwaji wa mahusiano ya kimapenzi bali huwa ni utayari wa nafsi.

Akizungumza kupitia kipindi cha DADAZ cha EATV kinachorushwa kila siku za Jumatatu hadi Ijumaa, hii leo Agosti 20, Padri. Fred Maziku ambaye pia ni mwanasaikolojia amesema, maandalizi ya kuingia kwenye Ndoa huanzia kwenye suala la kiuchumi na kifikra na kwamba, haisukumwi na umri au sababu nyingine zisizokuwa za msingi.

Padri. Maziku amesema, si sahihi kwa watu kuamua kuingia kwenye Ndoa kwa kigezo cha umri au kuiga kutoka kwa watu wao wa karibu, kwani kwa kufanya hivyo ni vigumu kuwa na amani katika ndoa.

Ndoa ni maandalizi hauhitaji kukurupuka tu, unahitaji maandalizi ya kiroho, kiuchumi na kuwa tayari kuishi maisha ya mume na mke katika hali zote”, amesisitiza Padri. Maziku.

Aidha, ameongeza kuwa, katika mahusiano, mwanamke hupenda polepole na kwa hisia zote tofauti na mwanaume ambaye hufikiria kufunga ndoa ili kupata mke huku mwanamke huwaza kupata watoto, hivyo asili ya mwanamke ni uhai.

Katika kipindi cha hivi karibuni mahusiano mengi yamekuwa yakishindwa kushamiri na kuvunjika muda mfupi baada ya ndoa kutokana na sababu ambazo mwanasaikolojia ameainisha ikiwemo kuoa au kuolewa sababu ya shinikizo kuhusu kitu au mtu wakati nafsi haijawa tayari.