Thursday , 4th Oct , 2018

Madeni ni jambo ambalo linawaumiza sana watu wengi, lakini sababu kubwa inayopelekea watu kuwa na madeni ni kuwa na matumizi matumizi makubwa kuliko kipato halisi.

Mtu aliyeelemewa na madeni kwa kiasi kikubwa hawezi kufanya shughuli zake za kimaendeleo na uzalishaji mali kwa uhuru kwasababu pesa ambazo anazizalisha huishia mikononi mwa wadai wake. Fahamu njia hizi kubwa tano zitakazokusaidia  kuepuka au kupunguza kiwango chako cha madeni.

Tengeneza vyanzo vingi vya mapato

Tatizo la watu wengi sana ni kutegemea chanzo kimoja cha mapato, mfano mtu anategemea ajira pekee katika kuendesha mipango ya maisha yake kiasi kwamba hata kukitokea na dharura ya kuchelewa kwa mshahara, basi mtu huyo atalazimika kukopa. Jijengee vyanzo vingi vya mapato ili kuweza kumudu katika changamoto kama hizo.

Anzisha benki yako

Wahenga waliosema 'Akiba haiozi' hawakukosea, kwani suala la kujitunzia akiba sio tuu humfanya mtu kujiamini anapokumbwa na matatizo ya kifedha bali hata kukusaidia katika kutengeneza mtaji wako ambao utakuwezesha kuanzisha vyanzo vingi vya mapato vitakavyokuingizia pesa.

Pasipo na ulazima 'acha'

Usiingie katika madeni kwa vitu ambavyo havina ulazima katika maisha yako. Mkurugenzi mmoja wa shirikisho la mabenki nchini Singapore, Ong-ang Ai Boon akiwahi kusema kuwa " Ni muhimu kwa wateja kukopa pale tu panapokuwa na ulazima wa kufanya hivyo ", hiyo itakusaidia kwa kiasi kikubwa kukimbia madeni.

Jibane

Kujibana katika hili inamaanisha kwamba mtu anatakiwa ajifunze kutumia kidogo kwenye kile anachokipata. Matumizi yasizidi maingizo yako, kwasababu endapo utaruhusu matumizi kuwa makubwa kuliko unachoingiza tambua baada ya muda mfupi utaanza kukimbizana na wadai wako.

Usidanganywe

Kila mtu ana marafiki wengi katika maisha, wanaweza kuwa ni marafiki wazuri au wabaya. Kutokana na hilo mtu anapaswa awe makini na marafiki anaopenda kutembea nao hasa katika matumizi, mfano katika mitoko mbalimbali, wapo marafiki wanaopenda kutumia sana pesa katika starehe. Mtu unatakiwa kuwa na msimamo katika vitu kama hivyo ili kufikia malengo yako.