Friday , 18th Jan , 2019

Utakubaliana na mimi kuwa ni mara chache sana kuona mashabiki wa soka Tanzania kupagawa na mchezaji tofauti na mshambuliaji kutokana na kiwango alichokionesha uwanjani.

Feisal Salum 'Fei Toto', wa kwanza (kushoto) akiwa na rafiki yake miaka 10 iliyopita.

Lakini inashuhudiwa kwa kijana Feisal Salum, maarufu kama 'Fei Toto' ambaye alizaliwa Januari 11, 1998 visiwani Zanzibar na kuanza kucheza soka ngazi ya chini kabisa kama ilivyo kawaida kwa wachezaji wengi wa soka barani Afrika, kabla ya kujiunga na klabu ya JKU msimu wa 2016/17.

Alijiunga na Singida United kwa mara ya kwanza mwezi Agosti msimu uliopita akitokea Zanzibar, na baadaye siku hiyo hiyo alisaini Yanga na kuzua sintofahamu kubwa kabla ya klabu hizo kukubaliana na kuruhusiwa kuichezea Yanga.

Kumbukumbu yake ya miaka 10 nyuma, alikuwa akicheza mchangani na marafiki zake, wakati ambapo alikuwa akipigania kuifikia ndoto yake inayoonekana hivi sasa katika klabu ya Yanga. Marafiki ambao hata leo akienda Zanzibar watamsimulia tuu namna ambavyo walikuwa kipindi hicho lakini ukweli ni kwamba ni watu tofauti.

Kwa umri wake wa miaka 21 sasa, amefanikiwa kuwapagawisha mashabiki wa Yanga, wakimpa majina tofauti tofauti kama 'Pass Master' na mengineyo kwa namna anavyotulia katika eneo la kiungo. Mahali ambapo kijana yeyote unahitaji kiatu cha kufunika mguu na soksi za kuokota tu kuweza kuianza na kuifikia safari hiyo.

Kinachowachanganya zaidi ni yale mabao yake ambayo mara nyingi hayatarajiwi, ameendelea kudhihirisha hilo katikati ya wiki hii ambapo aliifungia Yanga bao la tatu  kwenye ushindi wa 3-0 kwa staili hiyohiyo katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Mwadui FC katika uwanja wa Taifa.

Baada ya kumalizika kwa mchezo huo, mashabiki walijitokeza nje ya uwanja wakiimba kwa nguvu huku wakitaja jina la mchezaji huyo, ambaye hivi sasa amejihakikishia namba katika kikosi cha kwanza. 

Mengi yanatarajiwa kutoka kwake na ni hazina kwa klabu yake na timu ya taifa, lakini endapo atapewa nasaha sahihi za jinsi ya kulinda kipaji chake. Cha kutia faraja zaidi ni kuwa nahodha wa zamani wa Yanga na Meneja wa klabu hiyo, Nadir Haroub Cannavaro ndiye anayemlea mchezaji huyo mpaka sasa.