Saturday , 10th Jun , 2017

Mara baada ya John Bocco kuondoka ndani ya kikosi cha Azam FC, klabu hiyo imefanikiwa kunasa saini ya straika mpya Mbaraka Yusuph aliyekuwa akiitumikia klabu ya Kagera Sugar.

Mbaraka Yusuph aliyekuwa akiichezea Kagera Sugar akisaini Mkataba kujiunga na Azam FC, kulia ni Meneja Mkuu wa Azam FC Abdul Mohamed.

Mbaraka Yusuph ni straika chipukizi aliyetamba msimu uliopita wa 2016/17 ndani ya kikosi cha Kagera Sugar katika Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara ambapo amesaini mkataba wa miaka miwili ndani ya klabu hiyo.

Ujio wa Mbaraka klabuni hapo utarejesha matumaini ya kuimarisha safu ya ushambuliaji ambapo katika miaka ya hivi karibuni Azam FC iliwapoteza mastraika waliokuwa na makali, Kipre Tchetche na John Bocco, hivyo Mbaraka kwa kushirikiana na Waziri Jr aliyetua klabuni hapo hivi karibuni akitokea Toto African ambayo imeshuka daraja wanatarajiwa kutengeneza ushirikiano katika msimu ujao wa 2017/18.

Aliyekuwa Kiungo wa Mbao FC Salmin Hoza (kushoto) akikabidhiwa jezi ya Azam FC.

 

Awali mchezaji huyo alikuwa akiwaniwa na Yanga na tayari mazungumzo yalishaanza lakini Azam FC imefanikiwa kufanya kweli kwa kuwazidi kete wapinzani wao hao.

Licha ya kumpata Mbaraka, Azam FC pia imefanikiwa kupata saini ya kiungo wa Mbao FC ya Mwanza,Salmin Hoza.

Hoza aliyejizolea sifa kemkem msimu uliopita kwa kuonyesha kiwango bora akiwa na Mbao FC amejiunga na Azam FC kwa mkataba wa miaka miwili.

Hoza anakuwa amchezaji wa tatu kujiunga na Azam FC ndani ya wiki kutokea timu za kanda ya ziwa.