Thursday , 10th Aug , 2017

Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, leo inatarajiwa kushuka dimbani kuminyana dhidi ya KCCA katika mechi ya kirafiki itakayofanyikia Jijini Kampala, Uganda kwenye uwanja wa Phillip Omondi majira ya saa 10:00 jioni.

Baadhi ya wachezaji wa Azam FC.

Taarifa zilizotolewa na kikosi hicho ambacho kimeweka kambi yake nchini humo kwa takribani siku 10 kimesema kimejiandaa vizuri kuelekea mchezo huo wa leo ambao watautumia vizuri kwa ajili ya kujiandaa kuelekea msimu mpya wa ligi kuu Tanzania Bara unataotarajiwa kuanza Agosti 26 mwaka huu.

"Kikosi kipo vizuri kabisa katika kambi hiyo na Kocha Mkuu, Aristica Cioaba na benchi lake zima la ufundi, wamekuwa wakifanya kazi kubwa kukipika vilivyo kikosi hicho pamoja na kuwaunganisha wachezaji kimfumo na kiuchezaji", ilisema taarifa hiyo. 

Katika hatua nyingine, mshambuliaji mpya wa Azam FC Mbaraka Yusuph amesema licha ya kusajiliwa na Azam FC lakini ana mipango ya kwenda kucheza soka la kulipwa katika nchi za ughaibuni.

“Kufika Azam FC ni njia moja ya mimi kusonga mbele, hivyo nina mpango wa kucheza soka la kulipwa katika timu kubwa zaidi, ila hauwezi kwenda kucheza huko bila kujituma mazoezini pamoja na kwenye mechi, nina imani nitafika huko,” alisema Mbaraka.

Mbaraka Yusuph aliyesaini kandarasi ya miaka miwili na Azam FC akiwa ametokea katika timu ya Kagera Sugar.