Thursday , 31st Jan , 2019

Inaelezwa kuwa kocha wa Chelsea, Maurizio Sarri alijifungia pamoja na wachezaji katika vyumba vya kubadilisha nguo, mara baada ya kumalizika kwa mchezo wake dhidi ya AFC Bournemouth usiku wa jana.

Kocha, Maurizio Sarri na benchi la ufundi la Chelsea

Mchezo huo uliopigwa katika dimba la Vitality, ulishuhudia Chelsea ikipigwa mabao 4-0 na kuzidi kuweka shakani hatma yake katika mbio za kumaliza nafasi nne za juu.

Kwa mujibu wa maripota kadhaa wa vyombo vya habari nchini humo, akiwemo Michelle Owen anayefanya kazi na kituo cha Sky sports wameeleza kushangazwa na namna ambavyo mkutano wa kocha huyo wa Chelsea na wana habari baada ya mchezo ulivyochelewa.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Michelle aliandika kuwa katika uzofu wa kazi yake, hakuwahi kushuhudia mkutano baada ya mechi ambao ulichelewa kama huo ambao ulichukua takribani saa moja kabla ya kuanza.

 

Pia inaelezwa kuwa Sarri aliwaondoa makocha wake wasaidizi akiwemo Gianfranco Zola ili abaki na wachezaji wake, ambapo alizungumza nao kwa muda wa takribani saa moja.

Baada ya kupoteza mchezo huo, Chelsea imeshuka katika nafasi ya tano ya msimamo wa ligi, ikiwa na pointi 47 sawa na Arsenal iliyo katika nafasi ya nne baada ya kushinda mchezo wake wa Jumanne.