Tuesday , 3rd Feb , 2015

Mashindano maalumu yenye lengo la kutafuta mabondia watakaounda kambi ya Timu ya Taifa yanatarajiwa kufanyika Februari 9 hadi 14 uwanjua wa ndani wa Taifa jijini Dar es salaam.

Akizungumza na East Africa Radio, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Ngumi Tanzania BFT, Makore Mashaga amesema mpaka sasa wana mabondia 45 ambao waliwapata katika mashindano ya ngumi Taifa yaliyofanyika Mwaka jana ambao wapo kambini lakini wanatarajia kuwapunguza na kupata vijana 15 watakaounda kambi hiyo ya muda mrefu.

Mashaga amesema, kati ya mabondia hao 15 watagawanyika katika makundi mawili ambao 10 watakuwa katika uzito wa juu na watano watakuwa uzito wa kawaida ambao watashirikiana wote wawapo kambini katika kipindi chote cha mazoezi.

Mashaga amesema, kuna baadhi ya wachezaji ambao hawakushiriki katika mashindano ya ngumi Taifa ambao wataungana na kikosi cha mabondia 45 ili kuweza kuchagua wachezaji wazuri zaidi ambao wataweza kushiriki mashindano mbalimbali makubwa ikiwa ni pamoja na mashindano ya All African Games yanayotarajiwa kufanyika Septemba mwaka huu, nchini Kongo Brazzaville pamoja na Olimpiki yanayotarajiwa kufanyika 2016 nchini Brazili.