Monday , 22nd Jan , 2018

Winga mshambuliaji wa Chelsea Eden Hazard ametofautiana na mawazo ya kocha wake Antonio Conte ya kutaka kusajili mshambuliaji mpya katika dirisha dogo la usajili.

Hazard amesema haoni haja ya Chelsea kusajili mshambuliaji mpya kutokana na mfumo ambao timu hiyo inatumia kuruhusu winga au kiungo kutimiza majukumu ya mshambuliaji.

"Sidhani kama timu inahitaji kusajili mshambuliaji labda kama tunataka kucheza mipira mirefu ndio anatakiwa kuwepo mtu wa kusimama lakini kama tunaweka chini mpira na kucheza basi tuna Morata na Batshuayi wanaweza kufunga vizuri'', amesema Hazard.

Hivi karibuni Conte alinukuliwa akisema timu hiyo inahitaji mshambuliaji mrefu mwenye uwezo wa kufunga mipira mirefu ili asaidiane na Alvaro Morata.

Hazard mwenye miaka 27 ametolea mfano kikosi cha Man City kwa kusema, ''mfano mzuri unaona Man City inaweka mpira chini inacheza na washambuliaji wake Aguero na Jesus sio warefu lakini wanafunga''.