
Akizungumza hii leo ofisini kwake jijini Dar es salaam wakati alipokutana na wafanyakazi wa BMT kwa mara ya kwanza tangu ateuliwe na Uongozi wa juu wa BMT, Kiganja amesema, sheria namba 12 ya mwaka 67 na marekebisho yake namba 6 ya mwaka 71, zinaelekeza kazi mbalimbali za kufanywa, na wao kama watendaji wanapaswa kujua hilo.
Akizungumzia maagizo ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Majaliwa Kasim juu ya kuundwa sera mpya ya michezo itakayokuwa ya kisasa, Kiganja amesema anasubiri sera hiyo itungwe na wizara ya michezo na yeye atatengeneza sheria mpya za michezo ikiwa ndiyo kazi yake.
Waziri wa habari,sanaa, utamaduni na michezo Mh. Nape Nnauye alitengua nafasi ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa BMT Henry Lihaya na kumuagiza Mwenyekiti wa BMT Bw. Deonis Malinzi kuchagua katibu mkuu mpya.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za BMT wiki iliyopita katika kikao kilichohudhuriwa pia na Lihaya pamoja na mwenyekiti wa baraza hilo, Dioniz Malinzi,Nnauye alisema kuwa katibu huyo alishindwa kuvisaidia vyama vya michezo.
Alisema kuwa vyama vya michezo vina matatizo mengi lakini mtendaji mkuu huyo alishindwa kabisa kuvisaidia, hivyo alisema anaondoka naye ili akampangie kazi nyingine wizarani.
Kabla ya uteuzi huo Kiganja alikuwa Afisa Michezo Mkuu katika Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuanzia mwaka 2015 mpaka uteuzi wake ulivyofanyika.
Pia aliwahi kufanya kazi kama Afisa Mwandamizi Michezo wa Baraza la Michezo Tanzania na Afisa Michezo Mkuu katika Ofisi wa Waziri Mkuu.
Kijanja ana shahada ya kwanza ya elimu katika masuala ya Michezo na Utamaduni kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam