Wednesday , 11th Mar , 2015

Timu za Kiluvya United ya Pwani, Mbao FC ya jijini Mwanza, Mji Njombe kutoka mkoa mpya wa Njombe na Mji Mkuu (CDA) ya Dodoma zimepanda Ligi Daraja la Kwanza (FDL) baada ya kuongoza katika misimamo ya makundi yao ya Ligi Daraja la Pili (SDL).

Katika taarifa yake, Afisa habari wa shirikisho la Soka nchini TFF, Baraka Kizuguto amesema kwa kuzingatia Kanuni ya Ligi Daraja la pili, timu hizo zitacheza kusaka Bingwa wa ligi Daraja la Pili ambapo Mji Njombe itacheza na timu ya Kiluvya United Machi 14 mwaka huu katika uwanja wa Amani Makambako, na mchezo wa marudiano kufanyika Machi 18, uwanja wa Mabatini Mlandizi, Mkoani Pwani.

Kizuguto amesema, Mbao FC ya Mwanza watawakaribisha timu ya Mji Mkuu FC mchezo utakaofanyika kwenye uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, na mechi ya marudiano itachezwa Machi 18, 2015 katika uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.

Kizuguto amesema, fainali inatarajiwa kufanyika Machi 22 mwaka huu jijin Dar es salaam ambapo uwanja wa mchezo utatangazwa baadae kwa kuzikutanisha timu zilizopata pointi nyingi katika michezo hiyo miwili ya awali.