Monday , 22nd Feb , 2016

Klabu ya TP Mazembe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imeshinda kombe la Super Cup kwa mara ya tatu kwa kuinyuka Etoile du Sahel ya Tunisia.

Mlinda mlango wa klabu ya TP Mazembe Robert Kidiaba akishangilia baada ya ushindi walioupata dhidi ya Etoile du sahel ya Tunisia wikiend iliyopita.

Mazembe walipata ushindi wa 2-1 kwenye mechi hiyo iliyochezewa mjini Lubumbashi Jumamosi iliyopita huku mabao yake mawili yakiwekwa kamani na mshambuliaji kutoka Ghana Daniel Adjei dakika za 20 na 45 huku la wapinzani wao likifungwa na Mohamed Msekni.

Mabingwa wa Afrika Mazembe pia walishinda kombe hilo linalokutanisha mshindi wa Ligi ya Klabu Bingwa barani Afrika na mshindi wa Kombe la Mashirikisho mwaka 2010 na 2011.

Mazembe ilitwaa ubingwa wa ngazi ya klabu barani Afrika huku ikichagizwa na uwepo wa nyota wa kimataifa wa Tanzania Mbwana Samatta ambaye kwa sasa anakipiga katika klabu ya KRC Genk ya Ubeligiji.