Thursday , 29th Nov , 2018

Kocha mkuu wa klabu ya Yanga Mwinyi Zahera amesema hofu yake kuu kuelekea mchezo wa leo dhidi ya JKT Tanzania ni stamina ya wapinzani wao, akiamini kuwa wana mazoezi ya kutosha kiasi cha kuweza kuwapa wakati mgumu kwenye mchezo huo.

Mwinyi Zahera wa kwanza kulia akiwa na benchi lake la ufundi

"Kwenye maandalizi yetu tumezingatia aina ya timu tunayokwenda kucheza nayo ambayo ni JKT Tanzania ni timu yenye mazoezi sana hivyo na mimi nimewaandaa wachezaji kukabiliana na hilo'', ameeleza Zahera.

Zahera ameongeza kuwa imani yake ni kuwa wachezaji wakifuata yale yote aliyowafundisha basi mwisho wa dakika 90 watapata pointi tatu kwenye mchezo huo.

Mchezo huo utachezwa kwenye uwanja wa taifa lakini kuna utata kutokana na JKT Tanzania kuwa mwenyeji wa mchezo lakini awali aliomba kutumia uwanja wa Mkwakwani Tanga kama uwanja wake wa nyumbani kabla ya bodi ya ligi kubadili na kuwaambia wachezee uwanja wa taifa.

Yanga kwasasa ipo nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikiwa na alama 32 kwenye mechi 12 huku JKT Tanzania wakiwa katika nafasi ya sita na alama zake 19 kwenye mechi 13 walizocheza.