Wednesday , 18th May , 2016

Shirikisho la Soka nchini TFF limeitupilia mbali rufaa ya timu ya Azam FC juu ya kukatwa pointi tatu kwa kumchezesha mchezaji Erasto Nyoni katika mchezo wao dhidi ya Mbeya City.

Afisa habari wa TFF Alfredy Lucas amesema, kamati ilikutana na ikafanya marudio kwa kuangalia ripoti wa aliyekuwa kamishna wa mchezo ule na kubaini kwamba mchezaji Erasto Nyoni alikuwa na kadi tatu za kuonywa hivyo Azam FC wataendelea na adhabu.

Lucas amesema, Nyoni alionywa kwa kadi ya njano katika mchezo wa ngao ya hisani dhidi ya Yanga uliochezwa Agasti 22 Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ambapo kadi ya pili ya njano aliipata katika mchezo wa ufunguzi wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara uliopigwa Septemba 12 dhidi ya Prisons.

Lucas amesema, Nyoni alipata kadi ya tatu katika mchezo dhidi ya Coastal Union uliochezwa Machi 16 na siku nne baadaye wakacheza dhidi ya Mbeya City ambapo ndio mchezo waliomchezesha Nyoni kimakosa.

Lucas amesema, kwa sheria za soka hata kama mchezaji alipata kadi mbili za njano na katika michezo aliyocheza ndani ya mwezi mzima hakupata kadi akaja kupata katika mchezo wa mwezi uliofuata bado kadi zitahesabika ni tatu, hivyo kadi za Nyoni ni sahihi.

Kwa upande mwingine Lucas amesema, mchezo wa Fainali ya Kombe la Shirikisho Tanzania Bara utakaowakutanisha Yanga dhidi ya Azam FC uliotarajiwa kupigwa Juni 11 sasa utapigwa Machi 25 kama ilivyopangwa hapo awali.