Monday , 7th Nov , 2016

Mdau wa Soka nchini na aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Klabu ya Simba Mhina Kaduguda, ameibuka na kuuponda uongozi wa sasa klabu hiyo na kusema kuwa hautaki kushauriwa pale ambapo unakosea.

Mhina Kaduguda - Mdau wa Soka

Amesema jambo hilo linaweza kuigharimu timu hiyo katika safari yake ya ubingwa wa ligi kuu Tanzania Bara msimu.

Kaduguda ambaye pia amewahi kuwa kiongozi mkubwa wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) zamani ikiitwa FAT, amesema mara nyingi amekuwa akitoa maoni yake katika ameneo ambayo yeye kama kiongozi mzoefu anaona hayaendi sawa lakini uongozi huo umekuwa ukimpuuza na kumuona kama mkosoaji.

"Tatizo la uongozi huu wa sasa, ni kwamba hautaki kushauriwa, mtu akitaka kukosoa katika maeneo ambayo hayako sawa, wao wanaona kama wanasemwa, kwahiyo wanachotaka ni kuambiwa yale mazuri tu, lakini ukweli ni kwamba kuna matatizo mengi sana ndani ya klabu ya Simba"

Kwa upande mwingine, Kaduguda amewashangaa wapenzi na mashabiki wa Simba waliokuwa wanaamini kuwa Simba haitafungwa msimu kutokana na kiwango inachoonesha, ambapo amesema kuwa suala hilo haliwezekani huku akikumbushia na kujivunia rekodi aliyoicha klabuni hapo ya kutwaa ubingwa bila kupoteza wakati akiwa kiongozi.

Evans Aveva - Rais Simba SC

Ameongeza pia kuwa hadi sasa ni mapema sana kuitabiria timu yoyote ubingwa, na hata wale wanaosema kuwa Simba inakuwa bingwa wanajidanya.

"Kusema Simba hii hatafungwa ni makosa makubwa, na mimi nilijua kwa African Lyon lazima tutakwaa kisiki, nakumbuka wakati ule nachukua ubingwa bila kupoteza, miongoni mwa timu ambazo tulitoka sare ni African Lyon, tulitoka nao sare ya 1-1, tena tulisawazisha dakika za mwisho kabisa, kwahiyo hii haikuwa timu ya kubeza ingawa wengi jana waliingia kwa kujiamini na kuona kana kwamba wameshinda kabla a kucheza" Amesema kiongozi huyo maarufu kama Simba wa Yuda.

Kwa mara ya kwanza katika msimu huu, Simba jana walipoteza mchezo wao kwa kufungwa 1-0 na African Lyon katika uwanja wa Uhuru na kuvuruga rekodi yao ya kucheza mechi 13 bila kufungwa, na mechi 6 bila kuruhusu bao.