
Akiongea mbele ya waandishi wa habari Haji Manara amesema kuwa viongozi hao wa Yanga wanataka bodi ya ligi isitoe pointi kwa Simba kufuatia mchezaji Mohammed Fakih wa klabu ya Kagera Sugar kuchezeshwa katika mechi ili hali mchezaji huyo alikuwa na kadi za njano tatu.
"Leo mchana huu kunatembea taarifa iliyotolewa na klabu ya Yanga inayoonesha kuishinikiza bodi ya ligi kutokutenda haki juu ya rufani yetu dhidi ya klabu ya Kagera Sugar kwa kumchezesha mchezaji Mohammed Fakih aliyecheza dhidi yetu akiwa na kadi tatu za njano ambalo ni kosa kisheria. Taarifa hiyo ya Yanga iliyomnukuu Mjumbe wa kamati ya utendaji ya klabu hiyo Salum Mkemi aliyeoongea mbele ya waandishi huku akiwa na katibu mkuu wa klabu hiyo Charles Boniface Mkwasa iliitaka bodi kutokutoa points kwa Simba eti kwa kuwa hizo points zitawaathiri Yanga kwenye kutetea ubingwa wao ambao kwa sasa upo rehani, pia taarifa hiyo imeonesha Yanga wanao ushahidi kuwa Fakih ana kadi mbili za njano" alisema Manara
Mbali na hilo Manara aliweza kuweka msimamo wao kama Simba na kusema...
"Klabu ya Simba inawaambia viongozi wa Yanga wanayo mambo ya msingi ya kuwashughulisha, ikiwemo kutafuta mishahara ya wachezaji wao iliokwama kwa miezi kadhaa kama inavyoripotiwa mitandaoni na kwenye vyombo vya habari, pia waangalie namna bora ya kuurejeshea hadhi uwanja wake wa mazoezi wa Kaunda ili upate kuchezeka tena na siyo ulivyo hivi sasa, ambapo umegeuka kama bwawa la kufugia kambale, hii ni rufani ya Simba dhidi ya Kagera siyo wao Yanga" alisema Haji Manara