Tuesday , 27th Feb , 2018

Shirikisho la soka nchini TFF kupitia bodi ya ligi, imesogeza mbele mchezo wa ligi kuu kati ya wenyeji Mtibwa Sugar dhidi ya Yanga SC ambao awali ulipangwa kuchezwa Machi 3 kwenye uwanja wa Jamhuri Morogoro.

Bodi ya ligi imeeleza kuwa sababu ya kuahirisha mchezo huo namba 170 ni kutoa nafasi kwa Yanga kufanya maandalizi ya mchezo wake wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Township Rollers ya Botswana utakaopigwa Machi 6 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa bodi ya ligi Clement Sanga ambaye pia ni Kaimu Mwenyekiti wa Yanga SC amesema lengo ni kuona timu zinazowakilisha taifa zinafanya vizuri kwa kuzipa muda wa kutosha kufanya maanalizi ya mechi zao.

Yanga ilikata tiketi ya kwenda Raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika Jumatano iliyopita licha ya sare ya 1-1 na wenyeji, Saint Louis Suns United katika mchezo wa marudiano wa Raundi ya Awali Uwanja wa Linite baada ya kuwa na faida ya ushindi wa bao 1-0 nyumbani.

Yanga itakutana na Township Rollers ya Botswana ambayo iliitoa El Merreikh ya Sudan, mechi ya kwanza itachezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Machi 6 kabla ya kwenda Gaborone kwa mchezo wa marudiano, Machi 17.