
Uingereza imeweka rekodi ya kuwa na wachezaji wawili katika hatua ya nusu fainali ya mashindano ya tenisi ya Grand Slam kwa mara ya kwanza tangu mwaka wa 1977.
Wachezaji Johanna Konta na Andy Murray wameweka rekodi hiyo baada ya kutinga hatua ya nusu Fainali ya mchuano wa tenisi ya wazi ya Australia.
Konta ametinga hatua ya nusu fainali baada ya kumzima Zhang Shuai kutoka China seti mbili kwa sifuri 6-4 6-1.
Konta sasa amekuwa mwanamke wa kwanza raia wa Uingereza kufuzu kwenye hatua ya nusu fainali tangu Jo Durie mwaka wa 1983.
Kufuatia ushindi huo Konta anayekamata nafasi ya 47 kwa ubora atakutana na Mjerumani Angelique Kerber anayeshika nafasi ya 7 kwa ubora duniani, huku Serena Williams akicheza na Radwanska.
Kwa upande wake Andy Murray anayeshika nafasi ya pili duniani ametinga nusu fainali baada ya kumtupa nje David Ferrer kwa jumla ya seti tatu kwa moja 6-3, 6-7 6-2 6-3 na atakutana na Milos Raonic siku ya Ijumaa, huku Novak Djokovic akimkabili Roger Federer.
