Thursday , 13th Oct , 2016

Viongozi wa mchezo wa mpira wa kikapu nchini wametakiwa kuzingatia mambo muhimu yanayotakiwa kupatiwa wachezaji kabla ya kuanza kwa mashindano yoyote ya mchezo huo

Wametakiwa kuiga mfano katika mashindano ya kumuenzi Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere yanayofahamika kama Nyerere Cup yanayoendelea Jijini Dar es Salaam.

Mdau ambaye pia ni mchezaji wa mchezo huo Frank Simkoko amesema, mchezo huo umeendelea kupoteza hadhi yake kutokana na kutokuwa na viongozi wenye uwezo wa kuuongoza hali inayopelekea hata wachezaji kushindwa kujitokeza katika mashindano mbalimbali wakihofia uhaba wa miundombinu ya mchezo huo ikiwemo huduma ya kwanza kwa mchezaji pale anapopata matatizo akiwa michezoni.

Simkoko amesema, ukosefu wa viongozi wanaoufahamu mchezo huo kwa undani ndiyo chanzo kikubwa cha kuendelea kushuka kwa mchezo huo kwani viongozi wengi waliopo ndani ya chama hawaupendi mchezo huo na hata kupelekea vilabu kushindwa kujitokeza pia katika mashindano mbalimbali.