Thursday , 29th Nov , 2018

Mzunguko wa tano wa hatua ya makundi ya michuano ya klabu bingwa barani Ulaya umekamilika hapo jana kwa baadhi ya klabu zikifuzu hatua ya 16 bora klabu zingine zikiwa hazina matumaini kabisa ya kusonga mbele.

Picha ya Neymar (kushoto) akifurahia bao

Baada ya michezo ya jana, jumla ya timu 13 zimeshajikatia tiketi ya kufuzu hatua inayofuata ya 16 bora ya michuano hiyo zikiwemo, Juventus, Manchester United, Real Madrid, AS Roma, Manchester City na FC Bayern Munich.

Timu zingine zilizofuzu hatua hiyo ni AFC Ajax, FC Porto, Schalke 04, FC Barcelona, Atletico Madrid na Borussia Dortmund.

Lakini licha ya timu hizo zilizofuzu, baadhi ya timu vigogo zipo katika wakati mgumu wa kufuzu hatua ya 16 bora kutokana na kuwa na alama chache katika msimamo wa makundi yao. Timu hizo ni pamoja na AS Monaco ambayo ina alama moja pekee mpaka sasa katika kundi 'A', Totternham Hortspurs na Inter Milan zilizofungana kwa alama 7 katika kundi 'B' ambapo zinatakiwa zitoe timu moja itakayoungana na Barcelona katika hatua inayofuata.

Katika kundi 'C', vigogo wote watatu, Napoli, PSG na Liverpool hawana uhakika wa moja kwa moja wa kufuzu hatua inayofuata kutokana na kukaribiana alama, lakini Liverpool yenye alama 6 pekee, ikiwa na wakati mgumu zaidi kuliko wengine. Sasa zinasubiri michezo ya mwisho ili kujua hatma ya timu zitakazofuzu katika kundi lao.